Matthew 10

Isa Awatuma Wale Kumi Na Wawili

(Marko 3:13-19; 6:7-13; Luka 6:12-16; 9:1-6)

1 aNdipo Isa akawaita wanafunzi wake kumi na wawili, naye akawapa mamlaka juu ya pepo wachafu, ili waweze kuwatoa na kuponya kila ugonjwa na maradhi ya kila aina.

2 bHaya ndiyo majina ya hao mitume kumi na wawili: wa kwanza, Simoni aitwaye Petro, na Andrea nduguye; Yakobo mwana wa Zebedayo, na Yohana nduguye; 3Filipo, na Bartholomayo; Tomaso, na Mathayo mtoza ushuru; Yakobo mwana wa Alfayo, na Thadayo; 4 cSimoni Mkananayo, na Yuda Iskariote aliyemsaliti Isa.

5 dHawa kumi na wawili, Isa aliwatuma akawaagiza: “Msiende miongoni mwa watu wa Mataifa, wala msiingie mji wowote wa Wasamaria. 6 eLakini afadhali mshike njia kuwaendea kondoo wa nyumba ya Israeli waliopotea. 7 fWakati mnapokwenda, hubirini mkisema, ‘Ufalme wa Mbinguni umekaribia.’ 8 gPonyeni wagonjwa, fufueni wafu, takaseni wenye ukoma, toeni pepo wachafu. Mmepata bure, toeni bure. 9 hMsichukue dhahabu, wala fedha, wala shaba kwenye vifuko vyenu. 10 iMsichukue mkoba wa safari, wala kanzu mbili, wala jozi ya pili ya viatu, wala fimbo, kwa maana mtendakazi anastahili posho yake.

11 j“Mji wowote au kijiji chochote mtakapoingia, tafuteni humo mtu anayestahili, nanyi kaeni kwake mpaka mtakapoondoka. 12 kMkiingia kwenye nyumba, itakieni amani. 13 lKama nyumba hiyo inastahili, amani yenu na iwe juu yake. La sivyo, amani yenu na iwarudie ninyi. 14 mKama mtu yeyote hatawakaribisha ninyi, wala kusikiliza maneno yenu, kung’uteni mavumbi kutoka kwenye miguu yenu mtakapokuwa mnatoka kwenye nyumba hiyo au mji huo. 15 nAmin, nawaambia, itakuwa rahisi zaidi kwa miji ya Sodoma na Gomora kustahimili katika hukumu kuliko mji huo.

Mateso Yanayokuja

(Marko 13:9-13; Luka 21:12-17)

16 o“Tazama, ninawatuma kama kondoo katikati ya mbwa mwitu. Kwa hiyo mwe werevu kama nyoka na wapole kama hua.

17 p“Jihadharini na wanadamu; kwa maana watawapeleka katika mabaraza yao na kuwapiga kwenye masinagogi yao. 18 qNanyi mtaburutwa mbele ya watawala na wafalme kwa ajili yangu, ili kuwa ushuhuda kwao na kwa watu wa Mataifa. 19 rLakini watakapowapeleka humo, msisumbuke kufikiria mtakalosema, kwa maana mtapewa la kusema wakati huo. 20 sKwa sababu si ninyi mtakaokuwa mkinena, bali ni Roho wa Baba yenu atakayekuwa akinena kupitia kwenu.

21 t“Ndugu atamsaliti ndugu yake ili auawe, naye baba atamsaliti mtoto wake. Watoto nao wataasi dhidi ya wazazi wao na kusababisha wauawe. 22 uWatu wote watawachukia kwa ajili ya Jina langu. Lakini yule atakayevumilia hadi mwisho ataokolewa. 23 vWakiwatesa katika mji mmoja, kimbilieni mji mwingine. Amin, amin nawaambia, hamtamaliza miji yote ya Israeli kabla Mwana wa Adamu kuja.

24 w“Mwanafunzi hawezi kumzidi mwalimu wake, wala mtumishi hamzidi bwana wake. 25 xYatosha mwanafunzi kuwa kama mwalimu wake, na mtumishi kuwa kama bwana wake. Ikiwa mkuu wa nyumba ameitwa Beelzebuli,
Beelzebuli kwa Kiyunani ni Beelzebubu, yaani mkuu wa pepo wachafu.
je, si watawaita zaidi wale wa nyumbani mwake!

Anayestahili Kuogopwa

(Luka 12:2-9)

26 z“Kwa hiyo msiwaogope hao, kwa maana hakuna kilichofichika ambacho hakitafunuliwa, wala hakuna siri ambayo haitajulikana. 27Ninalowaambia gizani, ninyi lisemeni mchana peupe. Na lile mnalosikia likinong’onwa masikioni mwenu, lihubirini juu ya nyumba. 28 aaMsiwaogope wale wauao mwili lakini hawawezi kuua roho. Afadhali mwogopeni yeye awezaye kuiangamiza roho na mwili katika jehanamu.
Jehanamu kwa Kiyunani ni Gehena, maana yake ni Kuzimu, yaani motoni.
29Je, shomoro wawili hawauzwi kwa senti moja tu? Lakini hakuna hata mmoja wao atakayeanguka chini pasipo Baba yenu kujua. 30 acHata nywele za vichwa vyenu zote zimehesabiwa. 31 adHivyo msiogope; kwa maana ninyi ni wa thamani kubwa kuliko shomoro wengi.

32 ae“Kila mtu atakayenikiri mbele ya watu, mimi nami nitamkiri yeye mbele za Baba yangu aliye mbinguni. 33 afLakini yeyote atakayenikana mimi mbele ya watu, mimi nami nitamkana mbele za Baba yangu aliye mbinguni.”

Sikuleta Amani, Bali Upanga

(Luka 12:51-53; 14:26-27)

34 ag“Msidhani kwamba nimekuja kuleta amani duniani. Sikuja kuleta amani bali upanga. 35 ahKwa maana nimekuja kumfitini “ ‘mtu na babaye,
binti na mamaye,
mkwe na mama mkwe wake;

36 ainao adui za mtu watakuwa
ni wale watu wa nyumbani kwake.’

37 aj“Yeyote ampendaye baba yake au mama yake kuliko anavyonipenda mimi, hastahili kuwa wangu. Yeyote ampendaye mwanawe au binti yake kuliko anavyonipenda mimi, hastahili kuwa wangu. 38 akTena yeyote asiyeuchukua msalaba wake na kunifuata, hastahili kuwa wangu. 39 alKwa maana yeyote anayetaka kuyaokoa maisha yake atayapoteza, lakini yeyote atakayeyapoteza maisha yake kwa ajili yangu atayapata.

Watakaopokea Thawabu

(Marko 9:41)

40 am“Mtu yeyote atakayewapokea ninyi atakuwa amenipokea mimi, na yeyote atakayenipokea mimi atakuwa amempokea yeye aliyenituma. 41 anMtu yeyote anayempokea nabii kwa kuwa ni nabii atapokea thawabu ya nabii, naye mtu anayempokea mwenye haki kwa kuwa ni mwenye haki atapokea thawabu ya mwenye haki. 42 aoKama yeyote akimpa hata kikombe cha maji baridi mmoja wa hawa wadogo kwa kuwa ni mwanafunzi wangu, amin, nawaambia, hataikosa thawabu yake.”
Copyright information for SwhKC